Abstract:
Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu suala la uana na watafiti mbalimbali katika jamii za Kiafrika na ulimwengu kwa jumla. Jamii za kijadi na hata za kisasa zingali zinatumia semi zinazoshusha hadhi ya wanawake katika mawasiliano yao. Semi hizi zinatumiwa katika mazungumzo kwa kujua au kwa kutojua. Jambo hili limekuwa la kawaida kutokana na imani potovu ya jamii inayowachukua wanawake kama viumbe duni ikilinganishwa na wanaume. Ingawa tafiti zimefanywa kuhusu uana, hakuna utafiti wa kutosha uliofanywa moja kwa moja kuhusu, uchunguzi wa maana za semi zinazosawiri uana katika lugha ya Kiswahili. Ili kutimiza lengo kuu la utafiti, madhumuni yafuatayo yalitumiwa; kubainisha maumbo ya semi mbalimbali zinazosawiri uana katika lugha ya Kiswahili, kuchanganua maana kijamii za semi mbalimbali zinazosawiri uana katika lugha ya Kiswahili na kuchunguza jinsi utamaduni wa Waswahili unavyoumba maana za semi kiuana katika lugha ya Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili. Nadharia ya kwanza ni ya Uwezo Uume iliyoasisiwa na Robert Bly na kuendelezwa na Connell. Nadharia hii hubainisha nguvu na mamlaka yanayomilikiwa jinsia ya kiume hasa kutokana na utamaduni
wa jamii husika. Nadharia ya pili ni nadharia ya Maana Kijamii. Nadharia ya maana kijamii imekua kutoka kwa kazi ya mwanasaikolojia Lev Vygotsky. Nadharia hii hueleza kwamba maana kijamii hutokana na muktadha unaotawaliwa na elementi za kijamii kama vile lahaja, imani na tamaduni za jamii. Utafiti huu ulitumia muundo wa kimaelezo. Utafiti huu ulikuwa wa maktabani na wa nyanjani. Data za nyanjani zilikusanywa kwa kundi lingani ya wataalam sita katika Makavazi ya Kiutamaduni ya Kiswahili Mombasa. Data ya maktabani ilikusanywa na mtafiti aliposoma Kamusi ya methali ya Lulu za lugha iliyoandikwa na Wamitila na Riwaya ya Chozi la Heri iliyoandikwa na Matei. Idadi lengwa iliyotumiwa katika utafiti huu ni semi sitini. Utafiti huu ulitumia sampuli ya uchunguzi wa sampuli ya sensa na kolevu kukusanya data. Mbinu za
majadiliano na kundi lingani pamoja na usomaji wa nyaraka za maandishi zilitumiwa kukusanya data. Data za maktabani na nyanjani zilichanganuliwa kimaelezo kutegemea madhumuni ya utafiti. Mtafiti aliwasilisha data kutumia maelezo na majedwali. Matokeo ya utafiti huu yalibaini kwamba, maana ya kijamii za semi nyingi za methali na misemo inayosawiri uana, zinaegemea sana wanawake kwa upande wa uhasi na wanaume kichanya. Matokeo haya yana umuhimu katika taaluma ya isimu, hasa katika lugha na uana kwa kubainisha maumbo ya semi yanayosawiri uana katika lugha ya Kiswahili na kuchanganua maana zao kijamii. Data ambazo zilikusanywa zilimwezesha mtafiti kujibu maswali ya utafiti na kujaza mapengo yaliyoachwa na watafiti wa awali. Utafiti huu unatoa mchango kwa dafina na matumizi ya lugha katika isimu matumizi. Vilevile, imeonyesha jinsi maana inavyosawiriwa kijamii inavyojikita katika mawanda ya utamaduni. Mtafiti alitoa muhtasari, hitimisho na mapendekezo ya utafiti wa baadaye. Mtafiti anapendekeza kuwa, watafiti wa baadaye wachunguze suala la maana na uana kwa mtazamo wa tanzu mbalimbali za fasihi.